Back to top

USAFIRISHAJI DAWA ZA KULEVYA WANNE KORTINI MOSHI

29 March 2025
Share

Wakazi wanne wa Wilaya ya Same wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, wakidaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa jumla ya kilogramu 518.57.

Watuhumiwa hao, Nimkaza Mbwambo, Prosper Lema, Nterindwa Mgalle, na Stephanie Mrutu, walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ally Mkama.

Wakili wa Serikali, Julieth Komba, aliwasomea mashitaka kwa nyakati tofauti ambapo alidai kuwa, Machi 21, 2025, watuhumiwa hao walitenda makosa hayo katika kijiji cha Rikweni, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro.

Katika mashitaka, ilidaiwa kuwa mshitakiwa Nimkaza Mbwambo alikamatwa akisafirisha kilogramu 138.58 za dawa za kulevya aina ya mirungi, huku Prosper Lema naye akikamatwa akiwa na kilogramu 113.29. Pia, Nterindwa Mgalle alikamatwa akiwa na kilogramu 160.25 za mirungi, wakati Stephanie Mrutu alikutwa akisafirisha kilogramu 106.45 za mirungi.

Kwa mujibu wa wakili wa serikali, upelelezi wa kesi hizo bado haujakamilika. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 11, 2025 kwa kutajwa, na watuhumiwa wote wamepelekwa mahabusu.

Wakati huo huo, wakazi wawili wa Wilaya ya Same, Dorisiana Mchome na Aisha Mbaga, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same wakikabiliwa na shtaka la kusafirisha kilogramu 54.15 za dawa za kulevya aina ya mirungi.

Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Hozza. Inadaiwa kuwa, Machi 21, 2025, katika kijiji cha Rikweni, Dorisiana alikamatwa akiwa na kilogramu 17 za mirungi, wakati Aisha alikamatwa akiwa na kilogramu 37.15.

Wakili wa serikali, Michael Matowo, aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na Kesi imeahirishwa hadi Aprili 10, 2025 kwa kutajwa, na watuhumiwa wote wamerudishwa mahabusu. Hata hivyo,  mtuhumiwa Dorissian Mchome kosa lake linadhaminika isipokuwa wadhamini wake wameshindwa kutoa taarifa sahihi mahakamani ila dhamana bado ipo wazi.

Kuanzia Machi 19 hadi 25, 2025, Mamlaka ya Kudhibiti  na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilifanya operesheni maalum wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, ambapo  Interindwa Kirumbi, maarufu kama "Mama Dangote", ambaye anadaiwa kuwa kinara wa biashara ya mirungi, alikamatwa pamoja na wenzake. Aidha, jumla ya ekari 285.5 za mashamba ya mirungi zilibainika na kuteketezwa, hatua inayodhihirisha jitihada za serikali katika kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.