Back to top

VIJANA WA KIKE FEDHA MNAZOPATA MZITUMIE PIA KATIKA UWEKEZAJI

03 March 2025
Share

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Nishati,  Bi. Ziana  Mlawa ametoa rai kwa Vijana wa Kike kuwa fedha wanazopata watumie pia katika kufanya uwekezaji hali itakayowajengea uwezo  kujiamini zaidi ikiwemo katika maeneo ya kazi.

Bi. Mlawa ameyasema hayo alipokuwa akieleza kuhusu nafasi ya Msichana katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo nchini yatafanyika kitaifa mkoani Arusha.

" Pamoja na majukumu yetu tuliyokuwa nayo tukijiwezesha na sisi kwenye uwekezaji itatujengea sana kujiamini kwenye kufanya kazi, ukiwa na uhuru wa kifedha kujiamini kunaongezeka kwenye kazi yako." Amesisitiza Bi. Mlawa

Amesema Wizara ya Nishati inaitekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya "Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” kwa namna mbalimbali ikiwemo suala la usawa kwani katika Wizara watumishi wanawake wapo 82 na wanaume 145 na kueleza kuwa kwa uwiano huo anaamini kauli mbiu hiyo imefanyiwa kazi.

Ameongeza kuwa hata kwa viongozi wa Menejimenti ya Wizara ambayo idadi yao ni 12 wanawake ni watano na wanaume ni 7.