Back to top

VIJIJI 63 VYAFANYIWA MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI CHAMWINO

22 August 2024
Share

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Geophrey Pinda, amesema jumla ya Vijiji 63 kati ya Vijiji 73, vilivyokuwa katika mpango kwenye Wilaya ya Chamwino mkoa wa Dodoma, vimefanyiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Pinda amesema Vijiji 10 vilivyosalia viko katika mchakato wa kufanyiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika Wilaya hiyo ya Chamwino. 

Mhe.Pinda amesema hayo katika mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Mkwayungu wilayani Chamwino, wakati kilele cha hitimisho ya ziara ya siku nne ya Makamu wa Rais Mhe.Dkt Philip Isdori Mpango, kukagua miradi ya maendeleo kwenye mkoa wa Dodoma.

Kwa mujibu wa Mhe.Pinda, mpaka kufikia Disemba, 2024 vijiji vyote wilaya ya Chamwino vitakuwa  imeshafanyiwa mipango wa  matumizi bora ya ardhi na kusisitiza kuwa, kimsingi migogoro ya mipaka ya vijiji imetatuliwa kwa kiwango kikubwa.

"Mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji inaondoa changamoto kati ya mwananchi na mwananchi,wilaya na wilaya pamoja na changamoto nyingine za ardhi katika maeneo mengine". Amesema Mhe.Pinda.

Aidha, ameongeza kuwa, kiasi cha Tshs. 1.5 bil kimetengwa na kutumika kwenye mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika wilaya ya Chamwino.

Sambamba na hilo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema, 
vijiji 27 vimepimwa na kutayarishiwa vyeti  ya vijiji huku vipande vya ardhi vilivyotambuliwa kwa ajili ya kutoa Haki za hatimiliki za Kimila ( CCROs) ni 20,455.