Back to top

VIWANJA 4,150 VYAMILIKISHWA KUPITIA PROGRAMU YA UKWAMUAJI URASIMISHAJI

01 July 2024
Share

Jumla ya viwanja 4,150 vimemilikishwa katika mitaa 270 ya mkoa wa Dar es salaam, kupitia programu ya ukwamuaji urasimishaji pamoja na kliniki ya ardhi katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi 2024.

Programu hiyo imewezesha viwanja 55,034 kupangwa na vingine 6,824 kupimwa sambamba na elimu kutolewa kwa kamati za urasimishaji za mitaa 46 ambapo jumla ya viwanja 2,727 vinavyotakiwa kumilikishwa vimeibuliwa.

Hayo yamebainishwa leo mkoani Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipopokea taarifa ya utekelezaji zoezi la ukwamuaji urasimishaji katika jimbo la Ukonga Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mhe.Pinda, miradi ya urasimishaji katika Halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam ilianza kutekelezwa mwaka 2013 ambapo hadi kufikia mwezi Desemba 2023 jumla ya viwanja 565,690 vilikuwa vimepangwa ambapo viwanja 132,811 vilipimwa na viwanja 42,513 vilimilikishwa.

"Takwimu hizi zinaonesha kuwa, utekelezaji wa programu ya urasimishaji wa makazi yasiyopangwa ulikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kasi ndogo ya upimaji na umilikishaji wa viwanja vilivyopangwa" amesema Mhe.Pinda. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe.Timotheo Mzava ameishukuru serikali kwa kuwezesha ukwamuaji urasimishaji maeneo ya makazi holela kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki (LTIP) hasa ikizingatiwa zoezi hilo halikwenda vizuri siku za nyuma.