Back to top

Wafanyabiashara Arusha walalamikia changamoto cha mashine za EFD.

12 July 2019
Share

Wafanyabiashara Mkoani Arusha wamelalamikia matatizo yanayoendelea kujitokeza katika matumizi mfumo wa ukusanyaji wa Kodi kwa kutumia mashine za EFD ambazo wamesema licha ya  kuonekana kuwa na tija kwa upande wa serikali kwa upande wao zinawaumiza na kuwasababishia uhasama na serikali usio wa  lazima.

Wakizungumza katika kikao cha kujadili matatizo hayo  wafanyabiashara hao wamesema kadiri siku zinavyokwenda   changamoto zilizoko kwenye mashine hizo zinaongezeka na  wanapouliza hawapati majibu sahihi na wana hofu kuwa huenda  kuna tatizo ambalo ufumbuzi wake haujulikani ama zimehujumiwa  na wajanja  wachache.

Wakizungumzia malalamiko hayo baadhi ya mawakala wanaosimamia  mashine hizo pamoja na kukiri kuwa kuna matatizo wamesema asilimia kubwa yako nje ya uwezo wao kwani yanatokana na mfumo.

Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha Bw Faustine Mdessa amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto alizodai kuwa ni za kawaida amesema  pia baadhi ya wafanyabiashara bado wanakwepa kodi kwa makusudi.

Akizungumza baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote  Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya  Arusha Bw Gabriel Dakharo amesema inavyoonekana lipo tatizo  la msingi ambalo ufumbuzi wake ni kila upande kutimiza wajibu  wake. 

Pamoja na mfumo wa ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za  EFD kuonyesha mafanikio bado yapo malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wafanyabiashara ambayo kundi la wafanyabiashara  wanadai kuwa kuna wajanja wanazi hujumu huku mawakala wakidai  kuwa ni ujanja wa baadhi ya watu wanaotaka kuendelea kukwepa kodi.