Back to top

WANANCHI MIKESE KUNUFAIKA NA ELIMU YA FEDHA.

22 August 2024
Share

Wananchi wa Tarafa ya Mikese Mkoani Morogoro wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuwapitia elimu ya fedha ambayo inatolewa kupitia Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21 – 2029/30.

Elimu hio imekuwa na msaada mkubwa  katika Tarafa ya Mikese baada ya wananchi wa Kata hiyo kusumbuka kwa muda mrefu kutokana na baadhi ya watu wasio waaminifu kutoroka na fedha zao walizokuwa wanawekeza kupitia vikoba visivyo rasmi. 

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Fulwe, Kata ya Mikese, amekuwa akipokea kesi nyingi kuhusu waweka hazina wa baadhi ya vikundi kuondoka na pesa za wanachama hivyo anaamini elimu hiyo itakuwa mkombozi kwa wananchi wa kijiji cha Fulwe na Tarafa nzima ya Mikese katika suala zima la uwekezaji. 

Kwa upande wake, Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Jackson Mushumba, alisema kuwa umuhimu wa utoaji elimu  kwa wananchi ni kuhakikisha wanaachana na mikopo umiza pamoja  na kuwa na uelewa kuhusu taasisi zinazotoa mikopo na vitu vya kuzingatia wakati wa kuchukua mkopo.