Back to top

Wananchi wazuia msafara wa waziri kushinikiza kupatiwa maji safi.

21 July 2019
Share

Wananchi wa kijiji cha Ruaha wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wamezuia msafara wa waziri wa maji Profesa Makame Mbarawa uliokuwa ukielekea wilayani Malinyi na kuangua vilio mbele yake wakishinikiza kupatiwa maji safi na salama ambayo yametajwa  kuwa kero ya muda mrefu licha ya kuwa na mito mingi inayotiririsha maji mwaka mzima.

Wakizungumza kwa masikitiko mbele ya waziri Mbarawa wananchi hao wamesema wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya mlipuko yakiwemo kipindupindu huku wakimlalamikia mtaalamu wa maji ambaye amekuwa akiwazuia kuendelea na mradi wao walioubuni kwa ajili ya kupunguza ukali wa ukosefu wa maji

Kufuatia kero ya wananchi hao waziri Mbarawa amewataka wananchi wa wilaya ya Kilosa kuwa wavumilivu wakati serikali inafanya juhudi za haraka kumaliza kabisa kero hiyo ya maji
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Mikumi Joseph Haule amesema kata ya Ruaha ina wakazi zaidi ya elfu 35 na kumuomba waziri Mbarawa kuchukulia maanani ombi la wananchi hao huku waziri mbarawa akiahidi kutatua tatizo hilo mapema iwezekanavyo