Back to top

WATAALAM UIMARISHAJI MPAKA TANZANIA NA BURUNDI WAFIKA MTO MALAGARASI

21 November 2024
Share

Kamati ya Pamoja ya Wataalamu ya Uimarishaji Mpaka wa Tanzania na Burundi (JTC) imefika Mto Malagarasi ambao ni sehemu ya mpaka wa kimataifa kati ya nchi hizo mbili na kujionea hali halisi ya eneo hilo, ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya umoja wa Afrika kuwa ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.

Uamuzi wa kutembelea eneo hilo la mto Malagarasi ni sehemu ya programu ya kikao cha JTC kinachoendelea katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma.

Kikao hicho pamoja na mambo mengine kimepanga kutembelea katika Vijiji vya Bukililo na Nyakayenzi upande wa Tanzania na Kijiji cha Kamusha nchini Burundi.

Timu hiyo ya wataalamu kwa upande wa Tanzania imeongozwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Samwel Katambi, huku upande wa Burundi ukioongozwa na Meja Jenerali Mbonimpa Maurice.

Lengo la kutembelea mpaka huo wa kimataifa ni kuwezesha JTC Kuandaa bajeti na mpango kazi wa uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo mbili.

Kikao cha Pamoja cha Wataalamu (JTC) kimeanza siku ya jumatatu tarehe 18 Novemba 2024 na kinatarajia kumalizika siku ya ijumaa tarehe 22 Novemba 2024.