Back to top

"WATAALAM WOTE WAONDOKE MARA MOJA, WAJE WAPYA" BASHUNGWA

08 April 2024
Share

Waziri wa Ujenzi Mh. Innocent Bashungwa ameagiza kuondolewa kwa wataalam wote, wanaosimamia ujenzi wa Barabara ya Kibaoni - Sitalike, sehemu ya kwanza ya Kibaoni - Mlele (km 50) kwa kiwango cha lami kutokana na ujenzi wa mradi huo kusuasua na utekelezaji wake kuwa nyuma kwa asilimia 23.71.

Ameagiza kuondolewa kwa Wataalam wote wa Mhandisi Mshauri wa Mradi Kampuni ya Crown Tech,  Msimamizi wa Mradi kutoka Makao makuu ya TANROADS, Eng. Ramadhan Myanzi pamoja na Msimamizi wa Mradi Mkoa wa Katavi, Eng. Albert Laizer.

Bashungwa ametoa agizo hilo mkoani Katavi wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kibaoni, Mkoani Katavi mara baada ya kukagua mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 14.7 na kutoridhishwa na kasi ya usimamizi na utekelezaji wa mradi huo.

“Mtendaji Mkuu wa TANROADS ninakuagiza watumishi wote ambao wapo chini ya Crown Tech wanaosimamia mradi pamoja na Msimamizi wa mradi kutoka TANROADS wote waondoke mara moja waje wapya, Nataka hii kazi ifanyike usiku na mchana barabara hii ikamilike kama ilivyopangwa”, Waziri Bashungwa

Aidha, Bashungwa amebaini ubovu wa mitambo mingi ya Mkandarasi na amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kupeleka timu ya wataalamu kufanya ukaguzi wa mitambo iliyopo eneo la mradi na kutambua mingapi inafanya kazi na mingapi haifanyi kazi pamoja na kuchukua hatua za kimkataba kwa Mkandarasi na Mhandisi Mshauri.

Bashungwa amemuagiza Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kuanza kumkagua Mkandarasi CRSG ambaye amekuwa akisumbua katika miradi mingi pamoja na kufika katika mradi huo kuangalia kwa mujibu wa sheria kama anafaa kuendelea kupata kazi na hatua za kisheria zichukuliwe.