Back to top

WATAFITI WA MIMEA VAMIZI WATUA SERENGETI

21 February 2025
Share

Ziara ya kikazi ya watafiti wa mimea vamizi kutoka Jamhuri ya Cuba walioungana na wataalam wa Ikolojia kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti inatarajiwa kuwa neema kubwa kwa Wanyamapori kwenye Hifadhi hiyo, kwa kuongeza maeneo ya malisho kwa wanyama hao ambayo kwa sasa yameanza kuathiriwa na mimea vamizi.

Akizungumza na watafiti hao katika Hifadhi hiyo ya kipekee duniani, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Stephano Msumi ameushukuru na  kuupongeza uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua hiyo muhimu ya kuwakutanisha watafiti wa Wizara hiyo na kutoka nchi Cuba kutembelea Hifadhi ya Serengeti ili kujionea changamoto hiyo kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wakudumu.

Amesema kuwa Hifadhi hiyo ni moja ya Hifadhi za Taifa zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa kupitia utalii hususani wa Wanyamapori hivyo jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha Wanyamapori wanapata malisho ya kutosha ni za  kuungwa mkono. 

Ameongeza kuwa zipo juhudi zinazofanywa na wataalam kutoka katika Hifadhi hiyo za kupambana na mimea vamizi lakini bado hazijazaa matunda yaliyotarajiwa, hivyo uwepo wa watafiti hao kutoka Cuba na kuungana na watafiti wa Wizara hiyo ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya kuhakikisha malisho na usalama wa ikolojia ya Hifadhi hiyo ni endelevu.

Kwa upande wake mtaalam mtambuzi wa mimea asili kutoka nchini Cuba, Dkt. Ramona Oviedo Prieto ametoa ushauri kwa wataalam wa ikolojia  wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kuchukua hatua za haraka za kulinda kingo za Mto Mara uliopo ndani ya Hifadhi hiyo kwa kurejeresha mimea ya asili iliyokuwepo pembezoni mwa Mto huo.

Wakiwa kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti, timu hiyo ya watafiti walitembelea maeneo ya Seronera, Ikoma, Mto Mara na Machochwe na kushuhudia  mimea vamizi aina ya gugu karoti ( Parthenium hysterophorus) Chromolaena odorata na Opuntia ambayo ndio imeanza kusambaa kwenye maeneo hayo.