GEITA.
Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Geita imewakumu kunyongwa mpaka kufa watu wanne wakazi wa eneo la Katoro mkoani Geita kwa kukutwa na hatia ya kumuua kwa makusudi kwa kumkatakata kwa mapanga aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Geita na mgombea ubunge jimbo la Busanda marehemu Alphonce Mawazo aliyeuawa mwaka 2015 akiwa njiani akitokea kwenye kikao cha kuchagua mawakala eneo la kata ya Ludete.
Akisoma hukumu hiyo nambari hamsini na sita ya mwaka elfu mbili na kumi na tano Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Geita hakimu mkazi mwandamizi mwenye mamlaka ya ziada Frenki Mahumbari anasema mnamo tarehe kumi na nne ya mwezi novemba mwaka elfu mbili na kumi na tano marehemu Alphonce Mawazo akiwa kwenye moja ya shughuli za chama chake cha CHADEMA alivamiwa na watu wanne eneo la Katoro na kumkata kata kwa mapanga na kupelekea kifo chake.
Hakimu huyo mkazi mwandamizi amewataja watu hao kuwa ni Alphani Apolinari, Epafula Zakaria, Hashimu Sharifu na Kalunda Bwire kuwa Mahakama imewakuta na hatia kutokana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani na mahakama imejirishisha pasipo shaka kuwa walimuua kwa mapanga, marungu na moko marehemu Alphonce mawazo hivyo mahakama imetoa adhabu ya kifo kwa wahusika wote.
Nje ya Mahakama hiyo wakili mwandamizi wa serkali Hezroni Mwasimba pamoja na katibu wa CHADEMA mkoa wa Geita, Deogratius Shinyanga wakaipongeza mahakama hiyo ya kutenda haki kwa shauri hilo lililovuta hisia za wakazi wa mkoa wa Geita.