Back to top

WAZIRI MKUU: SUALA LA MAZINGIRA LIWE AJENDA YA KITAIFA

11 September 2024
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe ajenda ya Kitaifa na jukumu la kila mmoja kuanzia ngazi ya familia mpaka Taifa.
 
"Na tunapokwenda kuhifadhi mazingira lazima tuanze na ngazi ya familia na tunapopanda juu tupanue wigo hadi kwa wadau mbalimbali. Viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa na hii lazima iwe ajenda maalum, iwe ni ofisi za umma, za binafsi au kwenye taasisi"-Mhe.Majaliwa
 
Ametoa kauli hiyo, wakati akifunga mkutano maalum wa viongozi na wadau wa mazingira ulioitishwa ili kujadili mwenendo wa mazingira nchini. Mkutano huo ulifanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. 
 
Amesema kitendo hicho kitakuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuimarisha uhifadhi na Usimamizi wa mazingira nchini, kazi aliyoifanya kwa weledi, ustadi na mafanikio tangu akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo juu ya jitihada ambazo Rais Dkt. Samia amekuwa akizichukua ili kuhakikisha suala la nishati safi linakubalika.
 
"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuja na dhana mpya ya kukataa kukata miti na kutuhamasisha kuhusu nishati safi ya kupikia. Rais wetu amekuwa kinara wa nishati safi hadi na mwezi Mei alienda Ufaransa kuhutubia kuhusu nishati safi na yeye akiwa ni Mwenyekiti mwenza wa mkutano huo. Hii ni fahari kwa nchi yetu," amesema.
 
Amesema Serikali imetoa fursa kwa wajasiriamali kuanzisha biashara ya kuuza mitungi na majiko ya gesi hadi kwenye ngazi ya vijiji ili nishati hiyo iweze kupatikana kwa urahisi. “Huko mbele tutaweka ukomo wa matumizi ya mkaa na kuni"Ameongeza.
 
Katika kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa mazingira, Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua za kisera na kimkakati ili kuleta matokeo chanya.  

Amezitaja hatua hizo kuwa ni kuandaliwa kwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021; Kutungwa kwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2014; kuandaa na kutekeleza Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wa mwaka 2022 hadi 2032, kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2021 hadi 2026 na kutungwa kwa Kanuni na Miongozo inayohusu masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.