Back to top

WCF YAELEZA UTAYARI KATIKA ZAMA ZA AKILI MNEMBA

25 June 2024
Share

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, amewahimiza waajiri nchini kutumia mifumo ya TEHAMA kupata huduma zitolewazo na Mfuko huo ili kupunguza gharama na kuokoa muda.

Dkt. Mduma ameyasema hayo wakati akitoa salamu za Mfuko kwenye mkutano wa mwaka wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), ulioambatana na kongamano la wadau lililokuwa na kauli mbiu “Akili mnemba na mustakabali wa kazi/ajira: Uchambuzi kuhusu utayari wa Tanzania.

“Kwetu sisi suala la akili mnemba (artificial intelligence) tunaliona kama ni mwanga mwingine wa kutusaidia kuongeza ufanisi kwenye kazi zetu. Kwa sasa huduma zetu zote za usajili kwa waajiri, uwasilishaji wa michango, na utoaji wa taarifa kuhusu ajali au ugonjwa uliotokana na kazi zote ziko mtandaoni. Tunatarajia wengi wetu hapa na wajumbe wa ATE tayari mmeanza kuitumia,” Dkt. Mduma.

Aidha, Dkt. Mduma alisema WCF imekuwa mfano wa kuigwa katika huduma za fidia kwa wafanyakazi barani Afrika kutokana na idadi kubwa ya taasisi kutoka nje ya Tanzania kutembelea WCF kujifunza.

Akielezea faida za matumizi ya akili mnemba (artificial intelligence), Mkurugenzi Mkuu wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi.Suzanne Ndomba, alisema ni pamoja na kuongezeka kwa tija kazini, ufanisi katika kazi, huduma mahsusi na kurahisisha kazi mbalimbali.

Awali akifungua mkutano huo, Naibu Waziri – Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobasi Katambi amezihakikishia ushirikiano wa muda wote taasisi zote zilizo chini ya Ofisi hiyo, ukiwemo Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

 “Taasisi zote za Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kweli muendelee kupeana ushirikiano, Mhe. waziri Ndejembi amesema atahakikisha tunatoa ushirikiano wa kutosha muda wote usiku na mchana, sisi tupo tayari kufanyakazi ili kuhakikisha taasisi zinatekeleza majukumu yao na wananchi wanapata huduma kikamilifu,” alisema Mhe. Katambi.