Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi ametoa wito kwa Wizara ya Sheria na Katiba, pamoja na TLS, kushirikiana kwa maslahi ya taifa. Bw. Eliakim ametoa wito huo katika kikao kazi kilichowakutanisha Wizara, Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) na Kitengo cha Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu kwa lengo la kujengeana uwezo wa utekelezaji wa masharti ya Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu.
“Ili kulijenga Taifa la Tanzania kunahitaji ushirikiano baina ya Taasisi mbalimbali na ni jambo lisilokwepeka hivyo ni vyema kukaa kwa pamoja ili kujua majukumu ya kila mmoja katika kutafuta mustakabali wa kuzuia biashara hiyo. wapo baadhi ya watu wasiowaadilifu ambao wanaweza kushiriki kwa namna moja au nyingine katika utakatishaji fedha jambo ambalo halikubaliki Kisheria. ” Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi.
Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) Bi. Fatma Simba amesema mapambano dhidi ya biashara hiyo ni jambo linalohitaji nguvu ya pamoja kati ya pande zote na madhara ya utakatishaji wa fedha haramu ni ya Kiuchumi, Kijamii, Kisiasa na Kiusalama ambapo huhatarisha Utawala wa Sheria na Usalama.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Boniface Mwabukusi amesema TLS ni chombo cha Kisheria na Viongozi wake wameapa kuisimamia Katiba na Sheria na hawapo tayari kusimama kama kizingiti cha kuzuia utekelezaji wa jambo ambalo linaleta maslahi mema katika Taifa.