Back to top

"ZOEZI HILI LINAHITAJI USHIRIKIANO" MH. JACOBS

10 July 2024
Share


Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Tabora na Katavi, kuwa na ushirikiano kati yao, Serikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi.
 
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mh. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa Mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri, mkoani Tabora.
 
“Matokeo bora ya zoezi hili yanategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, Serikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegele.

Mafunzo hayo yamefunguliwa pia Mkoani Katavi na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mh. Asina Omari na yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 hadi 26, 2024.

Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.

Mapema kabla ya kuanza mafunzo hayo, washiriki walikula kiapo cha kujitoa uanachama na kile cha kutunza siri.

Tume imetangaza uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika Julai 20, 2024 mkoani Kigoma ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na kauli mbiu ya uboreshaji ni “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura ni Msingi Wa Uchaguzi Bora”.