Back to top

UBORESHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA ZANZIBAR KUFANYIKA OKTOBA 7.

30 September 2024
Share

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Zanzibar utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 07 hadi 13 Oktoba, 2024 ambapo vituo vitafunguliwa saa 02:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.

Akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi Kisiwani Pemba, Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk amesema uboreshaji huo wa daftari utajumuisha mikoa ya Mjini Magharibi, Unguja Kaskazini, Unguja Kusini, Pemba Kaskazini na Pemba Kusini.

Jaji Mbarouk amesema uboreshaji huo ambao unafanyika kwenye mzunguko wa sita kwa mujibu wa kalenda ya Tume kwa upande wa Zanzibar utahusu kuwaandikisha watanzania wote wanaoishi Zanzibar ambao wanastahili kuandikishwa kuwa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Akizungumza wakati akifungua mkutano kama huo Kisiwani Unguja, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari ameongeza kuwa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024, Tume itawaandikisha watanzania waliopo Zanzibar ambao wametimiza umri wa miaka 18 na zaidi au watakaotimiza umri huo wakati au kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Amefafanua kuwa mtanzania huyo atakeyandikishwa ni lazima awe hajapoteza sifa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi au sheria nyingine yeyote na awe anastahili kuandikishwa kuwa mpiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

“Kwa lugha nyepesi ni kwamba, Tume itamwandikisha mtanzania yeyote aliyopo Zanzibar ambaye amekosa sifa za kuandikishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Hivyo, atakayeandikishwa kwenye Daftari la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi atapiga kura moja tu ya kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Jaji Asina.

Uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari ulifanyika tarehe 20 Julai, 2024 mkoani Kigoma na mpaka sasa uboreshaji umeshafanyika kwenye mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Singida na sehemu ya mkoa wa Dodoma.