Baraza la Maadili limeanza kusikiliza malalamiko dhidi ya tuhuma zinazomkabili Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (TAA), Prof. Emilian Sedoyeka, anayetuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi hiyo, kinyume na kanuni na taratibu za maadili ya uongozi wa umma.
Akiwasilisha taarifa yake katika Baraza la Maadili dhidi ya tuhuma zinazomkabili Prof Sedoyeka , Wakili wa serikali Emma Gellan, amesema kiongozi huyo anatuhumiwa kwa kushindwa kutimiza matakwa ya sheria ya maadili ya umma kifungu cha 6(1)c na kifungu cha 12(1).vya sheria maadili ya uongozi wa umma.
Wakili Mkuu wa serikali Emma Gellan, amesema mlalamikiwa anatuhumiwa na mashtaka manne ikiwamo kumpandisha cheo Bw. Hakimu Ndatama, kutoka Afisa Rasilimali kuwa Mkuu wa sehemu ya rasilimali watu, kabla ya kukamilika kwa uhamisho wa mtumishi huyo na bila kuwa na sifa.
Hata hivyo wakili wa serikali amesema mlalamikiwa ana uhusiano wa karibu na Bw. Hakimu Ndatama kwa kufanya naye kazi Chuo cha Uhasibu Arusha, na Wizara ya Maliasili na Utalii, na aliporudishwa tena Bw. Hakimu Ndatama aliombewa ahamie Chuo cha Uhasibu Arusha na mara tu baada ya mlalamikiwa kuteuliwa kuongoza chuo hicho, ambapo amesema matendo hayo ni kinyume na kifungu cha sita moja.
Tuhuma nyingine anayokabiliwa nayo Prof.Sedoyeka ni kuingilia mchakato wa zabuni ya ununuzi na ufungaji wa viti na meza, katika kampasi ya Babati kwa kuifuta bila kufuata utaratibu na bila sababu za kisheria ziliainishwa, chini ya kifungu cha 59 2 cha sheria ya ununuzi wa umma sura ya 410.
Tuhuma nyingine ni kwamba mlalamikiwa wakati akitekeleza majukumu yake ya uongozi wa umma, alifanya uhamisho wa ndani wa mtumishi Bw. Robert Mwitango Afisa Ugavi kutoka kitengo cha ununuzi na ugavi, kwenda idara ya maktaba tofauti na sifa za kitaaluma za mtumishi huyo.
Baada ya kusomewa tuhuma zinazomkabili mlalamikiwa Prof Emilian Sedoyeka amekana tuhuma hizo zote nne zilizowasilishwa mbele ya baraza.