Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa amesema kuwa matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza la Mawaziri utasaidia kuboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.
Amesema hayo leo wakati akifunga Mkutano wa Kazi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri (e-CABINET), kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Amesema kuwa maboresho hayo ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya karatasi katika vikao vya Serikali, hususan Baraza la Mawaziri, hivyo kupunguza changamoto ikiwemo kuchelewa kwa taarifa, gharama kubwa za uchapaji na hatari ya upotevu wa taarifa muhimu.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa mkutano huo kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza la Mawaziri ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha kwamba Mawaziri na watumishi wa umma wanakuwa na ujuzi wa kisasa wa uendeshaji wa shughuli za Serikali na utumishi kwa ujumla.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kuwa uanzishwaji wa mfumo huo wa kielektroniki wa Baraza la Mawaziri ni utekelezaji wa Ibara za 102 na 103 za Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 zinazoelekeza Serikali kuhakikisha kuwa sayansi, teknolojia na ubunifu vinatumika kikamilifu katika kuendesha sekta za kukuza uchumi kwa lengo la kufikia uchumi wa hadhi ya kipato cha kati ambao ni shindani, jumuishi na unaoongozwa na viwanda.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Simbachawene amesema kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa mpango wa Serikali kwenda kwenye matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri (e-CABINET) mchakato ambao ulikuwa wa muda mrefu kupitia wataalam wa Wakala wa Serikali Mtandao.