Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo Dkt. Asimwe Rwiguza, amewataka wazalishaji, wauzaji na watunzaji wa vyakula vya Mifugo kufuata kanuni na taratibu zinazoongoza tasnia hiyo, kama zilivyoainishwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Ardhi na Rasilimali za vyakula vya wanyama sura namba 180.
Ameeleza hayo mara baada ya kukamilisha zoezi hilo ambapo ameeleza kuwa ameridhishwa na hali ya maghala ya makampuni ya Irvin na Silver land hususan kwenye eneo la miundombinu, mpangilio wa vyakula hivyo na udhibiti wa wadudu na wanyama wanaoweza kuathiri vyakula hivyo.
Amebainisha kuwa wizara ya Mifugo na Uvuvi na Halmashauri ya jiji la Dodoma imefanya ukaguzi kwa wazalishaji na wauzaji wa rasilimali za vyakula vya Mifugo waliopo Jijini Dodoma, na kushuhudia vyakula vya Mifugo vikiwa vimehifadhiwa juu juu ya kichanja ili kuzuia unyevunyevu kuathiri vyakula hivyo.
Akizungumza mara baada ya kukaguliwa na timu hiyo, Msimamizi wa ghala la kuhifadhi vyakula vya Mifugo la Irvin Bi. Emmaculate Edwin, mbali na kuipongeza Serikali kwa ukaguzi huo ameahidi kufanyia kazi yale yote waliyoshauriwa ili kuendelea kuboresha vyakula hivyo.
Naye Afisa Masoko wa kampuni ya Silverland kanda ya Dodoma Bi. Mwanawetu Rashid amesema kuwa zoezi hilo limewaongezea elimu ya uhifadhi wa vyakula vya Mifugo ikiwa ni pamoja na ushauri wa kuacha nafasi kati ya Ukuta na vyakula hivyo ili kuviepusha na unyevunyevu unaoweza kusababisha viharibike.
Zoezi hilo la Ukaguzi kwa wazalishaji na wauzaji wa rasilimali za vyakula vya Mifugo waliopo jijini Dodoma limefanyika kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau hao ili waendelee kulinda afya za walaji kupitia mifugo itakayotumia vyakula hivyo.