Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) Bw. Saleh Yahya, amesema Asasi mbalimbali za kiraia na Taasisi zisizo za Serikali zimekuwa na mchango mkubwa kwenye ukuzaji wa Tasnia ya Uvuvi mdogo nchini.
Bw. Yahya ameeleza haya wakati akifungua Warsha iliyoandaliwa na Kamisheni ya Bahari ya Hindi kupitia mradi wake wa EcoFish, ambayo imelenga kuangazia mchango wa Taasisi hizo katika kukuza Tasnia ya Uvuvi Mdogo kwa mataifa wanachama wa Kamisheni hiyo ikiwa ni pamoja na Tanzania.
Amesema "Sisi kama Tanzania kupitia Warsha hii tumejifunza namna ambavyo wadau wa sekta binafsi wanaweza kutusaidia kuendeleza Uvuvi Mdogo ambao kama mnavyojua unajumuisha takribani asilimia 90 ya Shughuli za Uvuvi unaofanyika nchini kwa ujumla" Ameongeza Bw. Yahya.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi kutoka Kamisheni ya Bahari ya Hindi (IOC) Bw. Marc Maminiana amesema kuwa warsha hiyo itawapa taswira ya namna ya kuunganisha majukumu ya Taasisi hizo zisizo za Serikali ili ziweze kuwa na tija na kuwa daraja kwa jamii ya Wavuvi wadogo na Serikali.
Akizungumzia manufaa ya warsha hiyo mwakilishi wa Shirika lisilo la Serikali la "CARDIO" kutoka Kenya Bw. Benedict Kiilu amesema kuwa matokeo ya warsha hiyo kwao ni pamoja na kuwasaidia kufanya shughuli zao kwa uwazi na kupitia ushirikiano watakaokuwa nao kuanzia sasa itawasaidia kuepuka kutekeleza miradi inayofanana kwenye jamii wanazozihudumia.
Pamoja na mambo mengine warsha hiyo imepokea na kujadili taarifa ya Mshauri Mwelekezi aliyefanya utafiti wa mchango wa Taasisi zisizo za Serikali kwenye sekta ya Uvuvi kwa mataifa yanayotekeleza miradi iliyopo chini ya Kamisheni ya Bahari ya Hindi (IOC).