Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaanza Mpango wa Utoaji wa Chanjo na utambuzi wa Mifugo Kitaifa kuanzia Mwezi Januari 2025 ambapo Shilingi Bilioni 28.1 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mpango huo unaolenga kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya mifugo nchini.
Haya yamebainishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Ashatu Kijaji, na kwamba mpango huo utakaotekelezwa kwa miaka mitano kutoka 2024-2029 na kugharimu Shilingi Bilioni 216 zitakazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Shilingi Bilioni 28.1, zitatumika awamu ya kwanza ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo kuanzia Mwezi Januari 2025.
Dkt. Kijaji amesema awamu ya kwanza ya mpango huo wa chanjo Serikali kupitia wataalamu wa Sekta ya Mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa itachanja ng’ombe 19,097,223 dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya ngo’mbe (CBPP), Mbuzi na Kondoo 20,900,000 dhidi ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (PPR) na Kuku wa asili 40,000,000 dhidi ya Ugonjwa wa mdondo wa kuku (ND) ambapo lengo la serikali ni kutoa chanjo kwa mifugo angalau asilimia 70 ya idadi ya mifugo husika kwa miaka mitano mfululizo.
Dkt. Kijaji amesema katika kufanikisha zoezi la chanjo ya mifugo serikali itachangia nusu bei ya gharama za chanjo ili kuwarahisishia wafugaji kuchanja mifugo yao.
Amehitimisha hotuba yake kwa kuwataka viongozi wa mamlaka ya serikali za mitaa, manispaa na majiji kutoa ushirikiano kwenye kampeni hiyo ya chanjo na kisha kueleza umuhimu wa chanjo za mifugo kwa taifa na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema Zoezi hilo la chanjo litahusisha wataalam na wafugaji katika kufanikisha hilo hivyo amewaomba wataalam na wafugaji kutoa ushirikiano wa zoezi hilo .
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Taifa CCWT Ndg. Mrida Mshota amesema zoezi la chanjo linalokuja kwa awamu hii litawasaidia mafugaji hasa kukabiliana na ugonjwa yaifugo na kuiomba Wizara kuupa kipaumbele pia ugongwa wa Miguu na midomo (FMD) na kisha kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania kuipa uzito na kipaumbele Sekta ya Mifugo.