Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kutekeleza Mradi wa usambazaji wa mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku, ambapo inatarajia kugawa mitungi 13,020 katika Mkoa wa Shinyanga, mradi huo utagharimu jumla ya shilingi milioni 545.538.
REA, iliingia mkataba na mtoa huduma; kampuni ambayo, itahudumia wilaya 4 za Mkoa wa Shinyanga kwa kuuza mitungi hiyo ya gesi ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku ya shilingi 20,950 pamoja na vifaa vyake, katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.
Hayo yameelezwa na Mhandisi Miradi wa Wakala wa Nishati Vijijini-REA Mhandisi Ramadhani Mganga wakati akizungumza na Wakunga, Wauguzi, kina mama waliojifungua watoto njiti na Mama wajawazito katika Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama na kuwagawia mitungi ya gesi ya Kilo sita kila mmoja ambapo jumla ya mitungi 100 imetolewa yenye thamani ya shilingi Milioni 4.1
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa REA Bi Martha Chassama amesema kuwa kazi ya Serikali ni kuhakikisha nishati safi za kupikia zinawafikia Wananchi wa vijijini kwa ukaribu zaidi na kwa bei nafuu na kuongeza kuwa Serikali inafanya kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga Mhe. Santiel Kirumba ameupokea mradi huo ambapo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele na kuipa REA fedha kwa ajili ya kuhakikisha wanawake wanatumia nishati safi na salama ambayo pia itaokoa muda na afya za watumiaji ikiwemo kuokoa mazingira.