Back to top

WANAOUZA NYENZO ZA UVUVI HARAMU KITANZINI

20 December 2024
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dk. Ashatu Kijaji, ameagiza kufungwa kwa viwanda na maduka yote yanayojihusisha na nyavu zisizofaa kwenye shughuli za Uvuvi ikiwa ni hatua ya kukomesha Uvuvi haramu nchini.

Mhe. Kijaji amesema hayo wakati wa ziara yake mkoani Mara, baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Uvuvi mkoani humo iliyobainisha kwa kiasi kikubwa changamoto ya uvuvi haramu.

Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha kuwa, atahakikisha anarejesha hali ya upatikanaji wa samaki nchini, kama ilivyokuwa awali ili kuokoa viwanda vya kuchakata samaki vilivyopo nchini na kudhibiti uingizwaji wa zana za uvuvi kwenye mipaka huku wakianza na mpaka wa Tunduma.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi, ametangaza awamu nyingine ya kupambana na uvuvi haramu mkoani humo, itakayoanza Januari mwakani, ambapo amewataka wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo, kuacha mara moja huku akiwatahadharisha kutomlaumu pindi atakapoanza kutekeleza operesheni hiyo.

Mhe. Dkt. Kijaji amefanya ziara yake ya kwanza kikazi mkoani Mara tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo ambapo amefanya vikao kazi na wataalam na watendaji wa Serikali mkoani humo na kutembelea vizimba vya kufugia samaki vilivyotolewa  na Serikali kwa mkopo wa masharti nafuu kwenye eneo la Lake Side.