Back to top

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KUHAMIA JENGO JIPYA MACHI 17.

11 March 2025
Share

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Eliakim Maswi amesema kuwa Wizara itaanza matumizi ya ofisi za jengo jipya ambalo lipo katika hatua za mwisho za ujenzi wake kwa kuhakikisha yeye mwenyewe akiwa ameambatana na timu ya Menejimenti inaanza kutumia jengo hilo ambalo mpaka sasa limefikia asilimia 86 ya ujenzi.

Katibu Mkuu Maswi amesema hayo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo la Wizara lililopo Mtumba jijini Dodoma huku akiwahimiza Mkandarasi SUMA JKT Kanda ya Mashariki kuongeza kasi zaidi ili kuendana na makubaliano ya mkataba wa ukamilishaji wa jengo hilo.

" katika kuendelea kuboresha utendaji kazi wa Wizara tumefanikiwa kupata Watumishi wapya na wapo Watumishi waliohamia hivyo uhitaji wa ofisi ni mkubwa sana. Nimeona ni vyema nianze mimi kuhamia nafikiri nikifanya hivyo kazi itakwenda kwa kasi mimi nipo tayari na kuanzia tarehe 17 Machi, 2025 kazi zangu zitakuwa katika jengo jipya" Alisema Maswi.

Kukamilika kwa jengo hilo jipya kunataraji  kuboresha mazingira ya utoaji Huduma za  Wizara na kuwezesha mazingira bora ya kazi kwa Watumishi.