Back to top

Serikali yataka masoko ya madini mikoa yote yenye madini ya dhahabu

31 March 2019
Share

Naibu waziri wa madini Stanslaus Nyongo ameagiza mikoa yote inayozalisha madini ya dhahabu nchini kuanzisha rasmi masoko ya madini katika ofisi za madini wakati taratibu za serikali zinaendelea sambamba na kumuagiza kamishna msaidizi wa madini wa wilaya ya Kahama kuandika barua ya kujieleza kwanini ameshindwa kutekeleza agizo la kuwafikisha mahakamani wahusika ambao walikamatwa wakikiuka maelekezo ya serikali .

Naibu waziri wa madini Stanslaus Nyongo ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika viwanda vya kuchenjua na kuchoma kaboni ya madini ya dhahabu na kugundua udanganyifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya matajiri wenye viwanda hivyo wakishirikiana na watendaji wa serikali katika sekta ya madini.

Kutokana na hali hiyo naibu waziri wa madini Stanslaus Nyongo ameagiza mikoa yote inayozalisha madini ya dhahabu kuanzisha masoko ya madini mara moja na kesho siku ya jumatatu yaanze kufanya kazi lengo ni kuzuia udanganyifu na utoroshaji wa madini.