Serikali ya Uholanzi kwa kushirikiana na Wadau wa Mifugo wanaandaa mradi utakaotumia teknolojia ya kisasa kuzalisha Chakula cha mifugo kwa wingi na kwa gharama nafuu ili kukabiliana na uhaba wa chakula cha mifugo hapa nchini.
Kauki hiyo imebainishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alipokuwa akifungua warsha iliyowakutanisha wazalishaji wa vyakula vya mifugo na wadau wengine ili kujadili namna ya kutumia mazao kama soya kuongeza Protini kwenye chakula cha Mifugo kwa lengo kutatua changamoto inayowakabili wafugaji wa Kuku na Samaki nchini.
Katika Warsha hiyo iliyoandaliwa na Ubalozi wa Uholanzi, Waziri Ndaki amesema kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Uholanzi katika kuhakikisha changamoto ya chakula cha mifugo inayokabili Wafugaji nchini inapungua.
"Sisi tunaunga mkono mradi huu na tunaamini endapo elimu ya kutosha itatolewa na Watanzania wakajitoa kikamilifu kutumia teknolojia hii mpya tunaweza tukafanikiwa kupunguza tatizo la lishe kwa kuku na samaki,"amesema Mhe. Ndaki
Aidha, Waziri Ndaki amewahakikishia wawekezaji wa vyakula vya mifugo wa ndani na kutoka nje ya nchi kuwa serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika eneo la uzalishaji wa chakula cha mifugo ili kukidhi mahitaji ya wananchi ambao wengi kwa sasa wanategemea kuagiza vyakula hivyo kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Fatma Nyangasa alisema teknolojia hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa wilaya yake na taifa kwa ujumla hasa ukizingatia kwamba wao pia wanafanya shuguli za uvuvi na ufugaji kwa ajili ya kuongeza kipato chao cha kila siku.
Kwa Upande wake, Mshauri wa Utafiti wa kuongeza Protini kwenye chakula cha mifugo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), Profesa Faustin Lekule ameeleza kuwa mpango wa mradi huo ni kuzalisha kwa wingi vyakula vya mifugo na kuingia kwenye viwanda ili kurahisisha upatikanaji.
"Kazi yetu sasa ni kuweka kwa pamoja mikakati ya kuzalisha kwa wingi vyakula hivi na vikipatikana kwa wingi itapelekea samaki na kuku kuwa chakula kinachopatikana kwa bei nafuu," amesema Prof. Lekule
Mkutano huo ulihudhuriwa na wazalishaji pamoja na wasambazaji wa chakula cha Mifugo kutoka Kenya na Tanzania.