Kila mwaka tarehe 16 Juni Tanzania inaungana na Nchi zingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.
Chimbuko la Maadhimisho haya ni Azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini waliouawa tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.
Watoto hao walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi. Kufuatia tukio hili, OAU iliazimia kuwa tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika.
Hivyo katika kuadhimisha siku hii ya mtoto wa Afrika, Mataifa, Jumuia mbalimbali na Jumuia za Kimataifa pamoja na wadau mbalimbali hukusanyika pamoja kwa ajili ya kujadili fursa na changamoto zinazowakumba watoto katika Bara la Afrika.
Siku hii ya mtoto wa Afrika inaadhimishwa kwa kuangalia maslahi mapana ya watoto wa Afrika na inawapasa watu wazima kujitolea kwa hali na mali katika nafasi zao ili kushughulikia changamoto nyingi zinazokabili watoto katika Bara zima la Afrika.
Watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya ukatili na unyama wanaoweza kutendewa ndani na nje ya familia zao. Vilevile Watoto wanapaswa kuepushwa na ndoa na mimba za utotoni kwa kupewa na kurithishwa maadili mema.
Katika siku hii na umuhimu wake, Wazazi wanapaswa kuwajibika kikamilifu juu ya ulinzi na tunza ya watoto wao kwani watoto wanapaswa kuepushwa na vishawishi vya aina yeyote ile kwa kuhakikisha kwamba, wanapata mahitaji yao ya msingi kwa wakati.
Pia wazazi wanahitajika kutenga wasaa ama muda wa kuzungumza na watoto wao kwa utuo na kwa lugha njema yenye kuhakikisha mtoto huyu anaona anaongea na mzazi na rafiki pia, ukali si sehemu sahihi ya kuhakikisha mtoto huyu anakaa katika maadili na hata kukua katika makuzi mema la hasha, mwalimu wa kwanza kabla ya darasa ni mzazi hivyo mzazi unapaswa kuketi na mtoto kumpa mwelekeo wa siku zijazo leo upo na kesho haupo afate misingi na maadili gani.
Watoto wafundishwe umuhimu wa kuwa na nidhamu katika maisha! Waswahili wanasema, watoto wakilindwa vyema, watawaheshimu na kuwakumbuka wazazi wao!
Tunakumbushana kuwa ili kuyafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, ipo haja ya kuhakikisha kwamba hakuna mtoto anayeachwa nyuma.
#Watotowanapaswakulindwa #SikuyamtotowaAfrika.