Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Samia Huluhu Hassan, ametekeleza ahadi ya Shilingi milioni 500 aliyotoa kwa Timu ya Taifa Stars, ikifuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023, nchini Ivory Coast.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu ambaye aliongoza msafara wa timu hiyo.
“Kubwa mtakumbuka wakati wa kujiandaa na mechi ya Uganda kule nyumbani Mhe. Rais alitoa ahadi ya kutoa Shilingi milioni 500, timu ikifuzu. Nafurahi kuwaambia kwamba hizo fedha sio tu kwamba zitatolewa, zimekwisha letwa Wizarani kwa ajili yenu”.Katibu Mkuu Bw. Yakubu.
Lakini pia kupitia ukurasa wa X.com, Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza Timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa kufanikiwa kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 baada ya kutoa suluhu na Algeria katika mchezo uliochezwa Uwanja wa 19 Mei 1956.
“Hongereni vijana wetu wa Taifa Stars kwa kufuzu michuano ya kuwania kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (2023 Africa Cup of Nations). Mmeandika historia kwani hii ni mara yetu ya 3 kufuzu tangu kuanzishwa kwa mashindano haya. Nawatakia kila la kheri.” aliandika Rais Samia.