Back to top

WALIOVAMIA HIFADHI BWAWA LA MINDU KUPATIWA VIWANJA

23 September 2023
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa, amesema Rais  Mh.Samia Suluhu Hassan , ameelekeza wananchi 357 wa Kata ya Mindu mkoani Morogoro ,waliovamia eneo la hifadhi ya bwawa la Mindu  kupatiwa viwanja.

Uamuzi huo unafuatia mgogoro wa muda mrefu baina ya wananchi na serikali , kufuatia Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 kutaka wananchi hao kuondolewa ili kulinda chanzo hicho cha maji.

Akizungumza na wananchi hao wakatI akifuatilia utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri, Silaa amesema, madai ya wananchi kuwa umbali wa mita 500 ulioanishwa kulinda eneo la bwawa la Mindu hayana ukweli kwa kuwa lengo la serikali si kujipatia eneo bali kulinda chanzo hicho cha maji.

Akielezea zoezi la uthamini lililofanyika, Waziri Silaa amesema hilo lilikuwa zoezi maalum ambalo lilibaini wananchi walioko ndani ya mita 500 wako kwenye eneo la hifadhi la bwawa la Mindu na kubainisha kuwa, hapo ndipo linapokuja suala la haki halali na ile haramu.

Kwa mujibu wa Waziri Silaa, fidia kwa wananchi waliovamia eneo la hifadhi ya bwawa la Mindu haipo, lakini kwa mujibu wa wataalamu wa ardhi wananchi 357 ndiyo wanaopaswa kulipwa kifuta jacho ikiwa ni huruma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kama mkono wa heri kuwasaidia kuhamisha mali zao.

Amesema baada ya kufanya mawasiliano na Rais Samia Suluhu Hassan alimuelekeza amuambie Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro awapatie viwanja wananchi wanaopisha uhifadhi wa eneo la bwawa ili waweze kujenga nyumba za kuishi.