Back to top

12 mbaroni kwa wizi wa maturubai Shinyanga.

25 May 2018
Share

Jeshi la polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu 12 kwa tuhuma za wizi wa maturubai ya magari makubwa ya mizigo yanayofanya safari kupitia barabara ya Isaka Kahama kupitia Lusahunga mkoani Kagera kwenda nchi jirani za Rwanda na Burundi huku mwingine mmoja akishikiliwa kwa tuhuma za matumizi ya dawa za kulevya aina ya mirungi.


Akithibitisha kukamatwa watuhumiwa hao na kushikiliwa na Jeshi la polisi kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Shinyanga ACP Simon Haule amesema watu hao wamekuwa wakifanya kazi hiyo nyakati za usiku kwa kutumia pikipiki zisizo na taa na njia nyingine ya kuwatumia wanawake wakijidai kama wanaomba lifti katika magari hayo.

Baadhi ya madereva wa magari ya mizigo ambao wamekumbwa na kadhia hiyo wametoa ushuhuda na kueleza namna wizi huo unavyofanyika nyakati za usiku huku baadhi ya wamiliki wa makampuni ambao wamefika katika kituo cha polisi cha Kahama na kutambua maturubai 34 yaloyofunguliwa na kuibwa katika magari yao.

Kufuatia matukio hayo Kamanda Simon Haule amewaonya wafanyabiashara na matajiri mkoani Shinyanga kuacha tabia ya kununua mali zinazoibwa na kuuziwa kwa bei ndogo mitaani mwao.

Watuhumiwa wanne waliokamatwa na kushikiliwa kwa tuhuma za kufungua na kuiba maturubai katika magari ya mizigo ni Daniel Juma, Philipo Osward,Emmanuel Bundala na Ngoya Samwel huku mtuhumiwa wa dawa za kulevya aina ya mirungi akitwajwa kwa jina la Munashri Shock Mohamed ambapo watuhumiwa 8 waliobaki majina yao yamehifadhiwa kwasababu za kiintelijensia.