Back to top

WHO YAIPONGEZA TANZANIA HATUA KUDHIBITI MARBURG

17 January 2025
Share

Shirika la Afya Duniani limeipongeza Tanzania kwa kuchukua hatua za haraka katika masuala ya afya mkoani Kagera, hasa ya ugonjwa unaoshukiwa kuwa ni wa Marburg, na kwamba WHO imepokea taarifa za hatua hizo ambazo ni muhimu kwa afya.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus, amesema serikali imepeleka timu ya taifa ya dharura, maabara zinazotembea, pamoja na vitengo vya matibabu kwa ajili ya kushughulikia hali hiyo, na kusisitiza utayari wake wa kutoa msaada wowote unaohitajika ili kuhakikisha changamoto hiyo inakabiliwa kikamilifu.

Amebainisha haya akizungumza na vyombo vya habari kwa njia ya mtandao kupitia Zoom, YouTube, na LinkedIn siku ya tarehe 16 Januari 2025, Dkt. Tedros ametoa muhtasari wa masuala ya afya duniani na kugusia hali ya afya katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania

WHO imeishauri Serikali ya Tanzania kuhakikisha sampuli zilizokusanywa mkoani Kagera, zinapelekwa kwenye maabara za rejea za kimataifa kwa uchunguzi wa kina, pamoja na kukusanya sampuli za ziada kwa kuzingatia taratibu za kawaida za afya ya umma.

Kadhalika imependekeza Serikali kuimarisha ufuatiliaji wa washukiwa wa ugonjwa husika kwenye mipaka ya mkoa huo, sambamba na kushirikiana na nchi jirani ili kuongeza uwezo wa kubaini na kutibu washukiwa wa ugonjwa huo.