Back to top

"WATANZANIA CHANGAMKIENI FURSA ZA AJIRA ABU DHABI"

15 January 2025
Share

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia umeme na nishati jadidifu Dk.  Khatibu Kazungu,  amekutana na kufanya mazungumzo na  Balozi wa Tanzania Abu Dhabi, Mh. Luteni Jenerali Mstaafu Yacoub Hassan Mohamed, alipokwenda kwenye ofisi za ubalozi huo kumtembelea.

Awali akizungumza kwenye kikao hicho Balozi wa Tanzania, Abu dhabi Luteni Jenerali Mstaafu Yacoub Hassan Mohamed alisema, Watanzania  wanapaswa kuchangamkia fursa za ajira zilizopo mjini Abu Dhabi kama ilivyo kwa nchi nyingine kama India, Kenya na Uganda ili kuinua uchumi wa nchi na kukuza kipato kwa wananchi wake.

Dk. Kazungu yupo mjini Abu Dhabi ambapo ameambatana na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Baraza la 15 la Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu IRENA, ambapo alimweleza Balozi Yacoub umuhimu wa Tanzania kupata fedha za kutosha kutoka kwa wawekezaji ili iweze kutekeleza miradi ya nishati jadidifu anbayo ni rafiki kwa mazingira na kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Tunaishukuru sana Serikali ya Mhe Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri inayofanya kutoa kipaumbele kwenye utekelezaji wa miradi na sisi kama Wizara ya Nishati tunaahidi kutekeleza kwa vitendo.” Alisema Dk. Kazungu.

Balozi Luteni Jenerali Mstaafu Yacoub Hassan Mohamed pia aliipongeza Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kazi nzuri inayofanya ya kuhakikisha umeme unakuwepo wa kutosha na wa uhakika hususani kwenye mradi wa treni ya mwendo kasi ambayo umekuwa na tija kwa wananchi na Serikali kwa ujumla

“Nitoe rai kwa Watanzania kuwa mabalozi wazuri wa mradi huu wa treni ya SGR pamoja na wataalamu wa TRC na TANESCO kuhakikisha wanafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha hakuna hitilafu yoyote na watanzania wafurahie matunda ya mradi huo kutoka kwenye Serikali yao.”

Katika hatua nyingine Dk. Kazungu alishiriki hafla ya ufunguzi wa  wiki ya uendelezaji nishati ikiwa ni mwendelezo wa fursa zilizopo kwenye Baraza Kuu la 15 la IRENA ili kutoa fursa za kubadilishana uzoefu na wawekezaji kwenye maonesho hayo.

Hafla hiyo iliambatana na  utoaji wa tuzo za Rais wa umoja wa falme za kiarabu UAE zijulikanazo kama  Zayed Sustainability Prize, kutambua mchango wa makundi mbalimbali yanayoleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya nishati ambapo mtanzania kutoka taasisi ya Open Map Development  ameshinda kwenye kipengele cha mabadiliko ya tabianchi.