Zaidi ya watu 700 wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani zilizotokea kati ya januari hadi julai mwaka huu, huku jumla ya watu 1,529 wakiwa ni majeruhi hali ambayo imesababisha taifa kupoteza rasilimali watu ambao ni tegemeo kubwa katika uzalishaji mali kuelekea uchumi wa kati wa viwanda.
Takwimu hizo zimetolewa na naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mhe. Hamad Masauni wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya siku ya mabalozi wa usalama barabarani yaliyofanyika jijini Mwanza, amewataka watumiaji wa barabara hususani madereva wa vyombo vya moto, yakiwemo magari, bajaji na bodaboda kuwa makini wakati wa kuendesha vyombo hivyo kwa kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani.
Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani nchini Fortunatus Muslim, amesema tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, wamefanikiwa kupunguza ajali kwa zaidi ya asilimia 30, huku kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Muliro Jumanne Muliro akiwataka askari kutimiza majukumu yao pasipo kumuonea mtu yeyote.
Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Mwanza Dkt.Philis Nyimbi ambaye ni mkuu wa wilaya ya Nyamagana, amesema mkoa huo unaendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, wakati mwenyekiti wa taifa wa taasisi ya mabalozi wa usalama barabarani John Seka akisema kwa kushirikiana na asasi nyingine za kiraia wataendelea kusimamia mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 ili kupunguza ajali za barabarani hadi kufikia asilimia 60.
Takwimu za ajali nchini zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2016 hadi julai 2019 kumetokea jumla ya ajali 20,683 zilizosababisha vifo 8,399 na majeruhi 19,722 kiwango ambacho ni kikubwa ambapo taifa limepoteza nguvu kazi, fedha na vifaa.