Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Afya imetoa dawa za kingatiba ili kudhibiti na kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambapo watu laki 257,358 kati ya watu laki 265,217 walipatiwa kingatiba kwa mwaka 2024.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maadhimisho ya kilele cha siku ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Duniani yanayoenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Tuungane. Tuchukue hatua. Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele”
Waziri Mhagama amesema kwa upande wa ugonjwa wa usubi, watu milioni 5,462,851 kati ya watu milioni 6,447,157 kutoka katika halmashauri ishirini na nne (24) walipatiwa kingatiba ya ugonjwa huo ikiwa ni sawa na asilimia 85, (kwa kipindi gani?)
“Watu milioni 1,603,425 kati ya watu milioni 1,967,143 kutoka halmashauri saba (7) za Ngorongoro DC, Monduli DC, Longido DC, Kiteto DC, Simanjiro DC, Mpwapwa DC na Kalambo DC, walipatiwa kingatiba za ugonjwa wa trakoma (sawa na asilimia 82), watoto wenye umri wa miaka 5-14 wapatao milioni 9,896,694 walilengwa kupatiwa huduma ya kingatiba kwa ugonjwa wa minyoo ya tumbo ambapo hadi kufikia Disemba 2024 Watoto 8,676,234 sawa na asilimia 88 walimeza kingatiba,” amefafanua Mhe. Mhagama.
Amesema upande wa ugonjwa wa kichocho walengwa wa kumeza kingatiba walikuwa watoto milioni 8,145,947 kati yao Watoto milioni 6,289,884 sawa na asilimia 77 walimeza kingatiba za ugonjwa huo ambapo walengwa hao walifikiwa katika halmashauri mia moja na sabini na moja (171) sawa na asilimia 93 ya halmashauri zote.
Ameongeza kuwa, mwaka 2024 watu wapatao 1,084 wamepatiwa huduma ya upasuaji wa mabusha, na takribani wagonjwa 2,412 sawa na asilimia 67 ya matarajio wenye tatizo la Vikope wamerekebishwa kope bila malipo.
“Nawapongeza watumishi wa Serikali na wadau wetu waliofanikisha mazoezi hayo kwa kazi nzuri ya kuhudumia Watanzania na kuwaepusha na maradhi kwani miongoni mwa malengo ya Serikali yetu ni kuendelea kutumia rasilimali chache zilizopo kudhibiti magonjwa yanayowasumbua wananchi wake,” amesema Mhe. Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imewekeza zaidi ya bilioni 38 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 kupitia mapato ya ndani, kwa lengo la kuendelea kutoa Huduma kwa wananchi za magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele zikiwemo utekelezaji wa Huduma za upasuaji wa matende na mabusha, usawazishaji wa vikope pamoja na utoaji wa dawa za kingatiba kwa jamii.
Shabaha ya utoaji wa kingatiba ni kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, hivyo Waziri Mhagama ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kujitokeza pindi mazoezi hayo yanapotangazwa kwenye maeneo yao.