Jeshi la polisi mkoa wa Dodoma limemkamata askari magereza Cosmas Ndasi wa gereza la Msalato jijini Dodoma akiwa na vipande sita vya pembe za ndovu zenye thamani ya shilingi milioni 103.5 akisubiri mteja kwa ajili ya kufanya biashara.
Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma SACP Gilles Muroto anasema askari huyo mwenye namba A.8070 Staff Sajenti amekamatwa na pembe hizo akiwa amezificha kwenye mfuko tayari kwa kufanya mauziano eneo la Kilimani jijini hapa.
Katika tukio jingine jeshi hilo linawashikilia Ambokile Mwampulo na Mohamed Hamis kwa nyakati tofauti wamejifanya maofisa usalama wa taifa na kujipatia fedha na mali kwa njia za udanganyifu kwenye taasisi za umma na watu binafsi yakiwemo magari mawili.
Kamanda Muroto amewataka wakazi wa Dodoma kujihadhari na wimbi la matapeli waliovamia jiji hili baada ya serikali kuhamia huku akionya polisi haitawaacha salama.