![](https://www.itv.co.tz/sites/default/files/styles/large/public/field/image/mwa_0.jpg?itok=aJsz_LR7)
Jeshi la polisi mkoani Pwani linamshikilia mkazi wa mtaa wa vitendo tarafa ya Misugusugu wilayani Kibaha mkoani Pwani fundi ujenzi Robison Ernest (33) kwa tuhuma za kumnyonga mtoto wake mwenye umri wa miezi sita Modesta Robison kwa madai kuwa sio mwanaye.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani ACP Wankyo Nyigesa amesema chanzo cha mauaji hayo ni baada ya mtuhumiwa kumtuhumu mkewe kuwa na mahusiano na mwanaume mwingine ambaye anamtuhumu kuwa ndiye baba halali wa marehemu mtoto huyo, hali hiyo ilipelekea mgogoro wa mara kwa mara kati yao na kusababisha tukio hilo.
" jeshi la polisi lilimuhoji mama mzazi wa marehemu mtoto huyo alitueleza kuwa mtuhumiwa aliwahi kufanya jaribio la kumuua mtoto wake kwa kumnyweshwa sumu ya vidonge lakini alimuwahi mtoto na mara ya pili alinoa panga amkate mtoto lakini hakufanikiwa pia mpaka tarehe 1/4/2019 ambapo mtuhumiwa alifanikiwa ku mnyonga mtoto hadi kufariki dunia," alisema kamanda.
Aidha alisema kwasasa wanamshikilia mtuhumiwa huyo na mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya rufaa ya Tumbi ya mkoa wa Pwani kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa taratibu za maziko.
Kamanda Nyigesa ametoa rai kwa wananchi wanapoona jambo la uhalifu,watoe taarifa mapema ili hatua ziweze kuchukuliwa kabla madhara zaidi hayajatokea na watuhumiwa wadhibitiwe.