Back to top

MSAADA YA KISHERIA WAFIKIA WANANCHI 161,154, GEITA

07 February 2025
Share

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign), imewafikia wananchi 161,154 katika Mkoa wa Geita ambapo kati yao wanaume ni 80,810 na wanawake ni 80,344.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Kampeni hiyo Mkoani humo, Wakili wa Serikali Candid Nasua wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kampeni hiyo kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Mohamed Gombati leo Februari 6, 2025.

Nasua amesema kuwa jumla ya migogoro 584 imepokelewa wakati wa Kampeni ambapo migogoro 86 imetatuliwa papo kwa papo na migogoro 498 inaendelea kushughulikiwa.

Kwa Upande wake Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Mohamed Gombati amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuifikisha Kampeni hiyo kwa wananchi wa Geita ambapo imekuwa na manufaa makubwa. 

Kampeni hiyo pia iliambatana na utolewaji wa huduma ya usajili, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambapo jumla ya wananchi 721 wamefikiwa na huduma hiyo, pamoja na uchangiaji wa damu salama, upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza, uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa kizazi na Uzazi wa Mpango.