![](https://www.itv.co.tz/sites/default/files/styles/large/public/field/image/DSJK.jpg?itok=lD5OqOls)
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Afya imefanya maendeleo makubwa katika kujenga uwezo wa kukabiliana na dharura za afya ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika mifumo ya afya, kuimarisha ushirikiano na wadau, kuanzisha mifumo ya tahadhari mapema pamoja na ufuatiliaji wa abiria na vyombo vya usafiri.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama, wakati akitoa wasilisho katika Mkutano wa 74 wa Mawaziri wa Afya wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati, na Kusini (ECSA – HC) kuhusu namna ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na masuala ya dharura za afya za umma katika kanda hiyo uliofanyika nchini Malawi.
"Magonjwa ya mlipuko yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na husababisha dharura za kiafya na kuhatarisha usalama wa afya za wananchi, Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuweza kukabiliana na dharura za afya na kuimarisha udhibiti dhidi ya magonjwa ya mlipuko” amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama amesema mnamo mwezi Machi mwaka 2023, Tanzania ilikumbana na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg kwa mara ya kwanza na ilifanikiwa kudhibiti kwa chini ya miezi mitatu, lakini pia hivi karibuni (Januari 20, 2025) mlipuko wa pili ulitokea na hatua zote za kudhibiti zilitekelezwa haraka na Tanzania ina uwezo wa kudhibiti mlipuko huo pia.
Vile vile, Waziri Mhagama ameweka wazi juu ya umuhimu wa kupitisha suluhu endelevu za uzalishaji wa huduma za chanjo, tiba pamoja na bidhaa za matibabu ili kukabiliana na tishio la afya ikiwemo kwa magonjwa ya milipuko.
Waziri Mhagama ameuambia mkutano huo kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano na Jumuiya ya Afya ya ECSA katika juhudi za usalama wa afya wa Kikanda na Kimataifa ambapo ameiomba Jumuiya hiyo kuendelea kushirikiana na Tanzania hasa katika kusaidia uratibu wa Chuo cha Madaktari wa Afya ya Umma (ECSA-COPHP).
“ushirikiano wetu wa kudumu wa kikanda unasaidia kuimarisha uwezo wa kushughulikia dharura jambo ambalo ni muhimu kwenye usalama wa afya ya jamii kwenye Jumuiya yetu" amesema Waziri Mhagama