Back to top

Familia ya Mwl.Nyerere yatoa pole nyumbani kwa Hayati Rais Dk.Magufuli

27 March 2021
Share

Familia ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere imemjulia hali Mama Janeth Magufuli kumpa salamu za pole kutokana na msiba wa aliyekuwa mume wake na Rais wa Tanzania Hayati Dk.John Magufuli.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Baba wa Taifa, Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere kutoka Ukoo wa Burito, Chifu Japhet Wanzangi amesema wameamua kwenda kutoa salamu za rambirambi kwa mama Janeth kutokana na kuguswa na msiba huo.

Chifu Wanzagi amesema salamu hizo za rambirambi wamezitoa zimeambatana na Ng'ombe dume mmoja kama sehemu ya kumtia faraja mjane wa Marehemu Mama Janeth Magufuli kulingana na mila na desturi za kabila la wazanaki linaloelekeza msiba ukitokea sehemu za utawala ni wajibu kutoa Ng'ombe dume.

Aidha Chifu wanzagi amewasilisha pia salamu za pole kwa mama Janeth Magufuli zilizotumwa na Mama Maria Nyerere ambaye amemtakia heri na nguvu ya ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu anachopitia.

Akishukuru baada ya kupokea salamu hizo za rambirambi Mama Janeth Magufuli ameeleza kufarijika na kupokea salamu za rambirambi zilizotolewa na mama Maria Nyerere na familia yote ya Nyerere na kusema  yupo pamoja na maombi, sala na dua za watanzania wote katika  kipindi hiki kigumu.