Back to top

Hekta 400 za miti katika shamba la Sao Hill zachomwa moto.

01 October 2018
Share

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga amesema atawachukulia hatua watumishi wazembe waliohusika kwa  kusababisha vibarua kutokulipwa mishahara yao  kwa wakati hali iliyopelekea hujuma za kuchoma shamba la miti lenye ukubwa wa hekta 400.

Ameyasema hayo mara baada ya kutembelea shamba la miti la Sao Hill kwa ajili ya kujionea hasara kubwa iliyosababishwa na moto uliotokea kwa muda wa siku nne mfululizo katika maeneo tofauti ya shamba hilo wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa Shamba hilo wilayani Mufindi mkoani Iringa.
 
Hujuma hizo za matukio ya moto zinadaiwa kupangwa na baadhi ya wafanyakazi wa muda (vibarua) wanaofanya kazi katika shamba hilo kutokana na kukosa mishahara yao kuanzia mwezi wa saba.

Kwa mujibu hasara hiyo iliyotokea,hadi hivi sasa  thamani halisi ya miti iliyoungua kwa ukubwa hekta 400 haijafahamika licha ya kuwa miti yenye umri wa miaka minne na yenye miaka kumi imeungua kwa moto kwa kiasi kikubwa.

Aidha,Mhe.Hasunga amesema katika kukabiliana na njama hizo,anatarajia kuunda tume itakayofanya kazi kwa muda wa mwezi mmoja ili kuwabaini watumishi wote waliofanya  njama hizo huku wakitaka mfumo wa kuwalipa vibarua kwa pesa taslimu urudi baadala ya mfumo mpya wa kuwalipa vibarua kwa benki.

Hatua hiyo inakuja kufuatia matukio ya moto ambayo yametokea kwa muda wa siku nne mfululizo kuanzia tarehe 25 hadi 28 Septemba mwaka huu.