Back to top

TANZANIA YAPOKEA MSAADA WA VIFAA TIBA KUTOKA CHINA

24 January 2025
Share

Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imetoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi milioni 125, vilivyokabidhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam ambao ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na China.

Wakati akipokea vifaa hivyo Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama, amesema kuwa msaada huo ni ushahidi mkubwa wa mshikamano imara na utayari wa pamoja katika kuimarisha huduma za afya nchini ili wananchi wapate huduma bora za afya.

"Msaada huu ni mchango muhimu sana katika kukabiliana na mahitaji ya huduma za afya kwa wananchi, pia katika kuimarisha ushirikiano na urafiki kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, hivyo tuendelee kudumisha umoja wetu ulioanzishwa na viongozi wetu hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong," amesema Waziri Mhagama

Waziri Mhagama ameutaka uongozi wa Hospitali ya Muhimbili kuvitunza vifaa hivyo, endapo vitaharibika wavitengeneze haraka ili viendelee kutumika ipasavyo katika kuimarisha utoaji wa huduma na kuleta matokeo chanya katika hospitali hii na wananchi waendelew kupata huduma bora za afya.

Aidha, Waziri Mhagama amesema Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeendelea kutuma timu ya wataalam wa afya nchini kila baada ya miaka miwili ambayo timu hiyo imekuwa msaada mkubwa sana katika hospitali zetu kwa kutoa mafunzo kwa ngazi ya ubingwa na ubingwa bobezi kwa wataalamu wetu wa ndani.

Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya watu wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Ming Jian amesema kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake, ikiwemo kutoa vifaa tiba ambapo hadi sasa wameweza kudumisha ushirikiano huo kwa zaidi ya miaka 60.

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amemshukuru Waziri wa Afya kwa kudumisha ushirikiano na watu wa china, "leo tunapopokea vifaa hivi vyenye thamani ya shilingi milioni 125 ni dhahiri kwamba ushirikiano huu unamanufaa makubwa sana Tanzania hasa katika Sekta ya Afya.