Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Upanga, kwa kushirikiana na taasisi ya ROAD2IR ya nchini Marekani, inatarajia kufanya kambi maalum ya uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa wenye maumivu makali ya viungo na sehemu mbalimbali za mwili, kwa njia ya kisasa ya tiba radiolojia itakayoongozwa na Daktari Bingwa Mbobezi wa matibabu hayo duniani Prof. David Prologo, kutoka Emory Health Care ya Marekani.
Dkt. Erick Mbuguje, Bingwa Mbobezi wa Tiba Radiolojia MNH amesema, kambi hii itahusisha matibabu ya wagonjwa wenye maumivu makali ya aina zote yaliyogawanyika katika makundi makuu mawili; maumivu ya mgongo na maumivu ya sehemu nyingine za mwili.
Tiba radiolojia ni aina ya taaluma ya matibabu ambayo daktari bingwa mbobezi hutumia teknolojia ya picha za uchunguzi za (Angio-Suite, CT, Xray, Ultrasound n.k) kumuongoza kufanya uchunguzi au tiba kupitia matundu madogo mwilini bila kufanya upasuaji.
Dk. Mbuguje amefafanua kuwa katika kundi la kwanza ni wagonjwa wenye maumivu makali ya mgongo yasiyosababishwa na saratani ni pamoja na pingili zilizosagika, kuvunjika au kupukutika ambapo matibabu ya maumivu hayo hayahusishi upasuaji, diski zinazokandamiza mishipa ya fahamu hivyo maumivu kusambaa sehemu za miguuni ambayo hayatibiki kwa upasuaji na wagonjwa wenye maumivu yatokanayo na maungio ya pingili na kuongeza kuwa kwa wagonjwa wenye maumivu ya mgongo yatokanayo na saratani iliyosababisha kuvunjika kwa pingili au kubana kwa mishipa ya fahamu nao watahudumiwa.
Dk. Mbuguje amesema kundi la pili ni wagonjwa wenye maumivu makali ya viungo vingine vya mwili ambayo hayajasababishwa na saratani kwenye magoti, mabega, nyonga ambayo matibabu ya maumivu hayo hayaondolewi kwa njia ya upasuaji na kuongeza kuwa katika kundi hili wenye maumivu mengine yatokanayo na saratani mbalimbali mfano kongosho nao pia watanufaika na huduma hiyo.
Huduma za uchunguzi na matibabu zitafanyika kuanzia tarehe 4 hadi 15 Novemba, 2024, Idara ya Radiolojia iliyopo karibu na jengo la Utawala, chumba namba 24, saa 02 asubuhi hadi 11 jioni na zitatolewa kwa utaratibu wa kawaida wa hospitali.