
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora Hussein Sadiki, ameumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya jeshi la Polisi kituo cha Nanga na wananchi waliouziwa viwanja ndani ya eneo la jeshi hilo katika wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora.
Kamishna Husein Sadiki na timu yake wamefika katika eneo la mgogoro kwa lengo la kukutana na uongozi na wajumbe wa serikali ya Kijjji cha Nanga, Mkuu wa kituo cha polisi Nanga pamoja na mtendaji aliyekuwepo wakati wa kubariki uuzwaji maeneo ya jeshi la polisi.
Mgogoro wa eneo hilo ulizuka kufuatia wananchi kuuziwa viwanja katika eneo la Polisi kwa madai kuwa uuzwaji huo ulibarikiwa kwa pamoja na uongozi wa kijiji cha Nanga pamoja na Ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Igunga.
Akizungumza katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro huo, Diwani wa kata ya Nanga Roberth Jidai amesema, yeye kama mwakilishi wa wananchi alipelekewa hoja ya kuwa wananchi wameuziwa viwanja kwa kufuata taratibu zote lakini wanazuiwa kufanya maendelezo kwa maelezo kuwa eneo hilo ni la jeshi la polisi jambo lililosababisha yeye kutaka kujua zaidi kuhusu suala hilo.
Amesema, baada ya kufuatilia kwa undani kwa kuiuliza serikali ya kijiji alielezwa kuwa, uuzwaji viwanja ni mradi wa serikali ya kijiji na ulibuniwa kwa lengo la kuupanga mji sambamba na kupunguza maeneo ya taasisi yaliyo makubwa na mpango huo ulishirikisha taasisi husika ikiwemo jeshi la polisi.
Kufuatia maelezo ya uongozi wa kijiji pamoja na kukagua baadhi ya nyaraka za mauziano ya viwanja, kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Tabora alibaini kwamba, kijiji kilikaa kikao kwa madhumuni ya kumega maeneo ya umma. eneo la Polisi lilimegwa na kutolewa vipande 51 vya ardhi. Upimaji wa vipande hivyo haukupata idhini na hakukuwa na mpango mji ulioidhinishwa. Aidha, baadhi ya wajumbe walikiwa ni wanufaika wa mpango huo.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora Hussein Sadiki, amewaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa, kikao kilichofanya maamuzi ya kuchukua na kuuza viwanja eneo la polisi hakikuwa na mamlaka hayo na kilichofanyika ni batili.
Mtendaji wa kijiji cha Nanga Henry Masanja alisema, kufuatia kadhia iliyotokea kuhusu uuzwaji viwanja aliomba mamlaka zenye jukumu la kusimamia mamlaka zilizo chini kuhakikisha zinatoa ushauri mzuri kwa mamlaka za chini kwa kuwa kilichotokea ni ushauri mbaya kutoka mamlaka ya juu.
Mjumbe wa serikali ya Kijiji Lawrence Kishiwa ameeleza kuwa tatizo ni wajumbe wanaochaguliwa kutopewa elimu ama semina kuhusu miiko na mipaka yao ya utendaji kazi kwa sababu wao wanaelezwa kuwa, wanayo mamlaka ya kugawa ardhi jambo alilolieleza linasababishwa na ukosefu wa elimu kuhusu utendaji katika mamlaka wanazozisimamia.
Aliyekuwa mtendaji wa kata ya Nanga Ambele Mwangomo ambaye alialikwa katika kikao hicho kutokana na kuwa kiongozi wakati wa zoezi la uuzwaji viwanja alieleza mbele ya kikao hicho kuwa, amejifunza viongozi wa serikali wanaoshirikiana na wananchi katika kutoa huduma kwa jamii wanapaswa kufuata misingi vizuri na sheria inavyoelekeza.
Akihitimisha kikao hicho, kamishna wa ardhi msaidizi mkoa wa Tabora Hussein Sadiki amesema, ni lazima viongozi wajionye katika nafsi zao hasa pale wanaposhughulika na mali za serikali. Ni hatari iwapo viongozi mliopewa dhamana mnabariki kumega na kujigawia maeneo ya umma. Ni batili. Kazi tunayoenda kuifanya ni kupitia kila mmoja anaesemekana alipatiwa eneo hili.