Back to top

Korosho za Mtwara, Lindi na Ruvuma kusafirishwa kupitia bandari.

06 June 2021
Share

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameagiza korosho zote zinazozalishwa katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi zisafirishwe kupitia bandari ya Mtwara kwani serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika bandari hiyo kwa kuikarabati na kuipanua.

Amesema hayo wakati wa kikao na wadau wa zao la korosho kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Sea View, iliyopo mjini Lindi ambapo amewaagiza viongozi wa bandari wapitie tozo zote zinazowakwaza wasafirishaji ili kuwavutia kuitumia bandari hiyo.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa wakulima wakubali kupokea pembejeo kulingana na mahitaji yao na watalipia kulingana na idadi ya mifuko waliyochukua na sio shilingi 110 kwa kila kilo kama inavyelezwa “kila kilo ni gharama mno, lengo letu ni kuendelea kumpungumzia mzigo mkulima, msiogope kuchukua pembejeo”

Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakulima wa zao la Korosho kuwa na utaratibu wa kubangua korosho ili kupata faida zaidi badala kuziuza bila kuzibangua.

Akiongelea tozo ya unyaufu, Waziri Mkuu amesema kuwa tozo hiyo haikubaliki kwa kuwa haina uhalisia kwani hata sheria na kanuni kwenye Wizara ya kilimo haitambui unyaufu.