Back to top

Mabula ampa mwezi kamishna wa ardhi kushughulikia migogoro Songwe.

19 July 2021
Share

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula amemuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Songwe Suma Mwakasitu kwenda katika wilaya ya Songwe kushughulikia migogoro ya ardhi ndani ya mwezi mmoja.

Hatua hiyo inafuatia Naibu Waziri Mabula kubaini uwepo wa migogoro mingi ya ardhi ambayo baadhi yake aliipata fursa ya kuisikiliza akiwa katika ziara yakeya kikazi wilayani Songwe kusikiliza na kuipatia ufumbuzi migogoro ya ardhi.

Dkt Mabula ambaye yuko katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye mikoa mbalimbali nchini alimtaka Kamishna wa Ardhi  mkoa wa Songwe kwenda na timu yake katika wilaya hiyo ili ikazipatie ufumbuzi changamoto za ardhi ambazo Naibu Waziri wa Ardhi hakupata fursa ya kuisikiliza na kuipatia ufumbuzi katika mkutano wake.

Alisema, hayuko tayari kuagiza mambo ambayo hayatekelezwi hivyo alimtaka Kamishna kukaa kwenye wilaya hiyo ya Songwe na timu yake katika kipindi cha mwezi mmoja na kuitafutia ufumbuzi migogoro yote ya ardhi katika wilaya hiyo.