Back to top

Mahakama yasikiliza ushahidi kesi ya mauaji kwa njia ya Video.

12 July 2019
Share

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba leo kwa mara ya kwanza imesikiliza kwa kutumia teknolojia ya mfumo wa video katika ushahidi wa kesi ya mauaji inayomkabili mkazi wa Mwanza Peter Kunambi maarufu kwa jina la Mkulya dereva wa basi la Complex Express anayetuhumiwa kumuua kikatili Grace Edward na kumtelekeza ndani ya chumba cha nyumba ya kulala wageni ya Michigan iliyoko katika manispaa ya Bukoba.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Mhe.Jaji Ntemi Kilekamajenga aliyetoa ushahidi ni afisa wa ofisi ya mkemia mkuu wa serikal,I domician Dominic aliyepima vielelezo vilivyowasilishwa na jeshi la polisi vinavyohusiana na kesi hiyo ambavyo ni pamoja na viroba na dawa yenye viambata vya sumu iliyokutwa ndani ya chumba hicho pamoja na mpanguso kutoka kinywa cha marehemu na mpanguso wa damu kwenye kinywa.

Akitoa ushahidi wake kwa njia ya video Dominic akiwa jijini Dar Es Salaam huku akiongozwa na Mwanasheria wa serikali Emmanuel Kahigi aliyekuwa mahakamani hapo amesema vielezo viwili kati ya vielelezo nane vilivyowasilishwa na jeshi la polisi na kufanyiwa uchunguzi kuwa ndivyo havina mahusiano na kifo cha marehemu.

Akizungumza shahidi huyo amesema uchunguzi umefanyika kwa umakini mkubwa hivyo akaiomba mahakama ipokee taarifa ya uchunguzi iliyowasilishwa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi kauli ambayo imepingwa vikali na Jackline Mrema wakili wa kujitegemea anayemtetea mtuhumiwa huyo aliyeiambia mahakama kuwa uchunguzi una mapungufu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 16, mwaka huu Mhe.Jaji Kilekamajenga atatoa maamuzi madogo kama mtuhumiwa huyo ana kesi ya kujibu, tukio hilo lilitokea Januari 4, 2016.

Baada ya kesi hiyo kuaihirishwa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe.Joyce Minde akizungumza amesema utaratibu wa kutumia video katika kutoa ushahidi utachangia kupunguza mlundikano na mashauri mahakamani na utapunguza gharama za kuwaita mashahidi.