Back to top

Mgomo wa machinjio wasabaisha uhaba wa nyama jijini Dodoma.

06 April 2019
Share

Wafanyakazi 125 wa machinjio ya mifugo Dodoma wamegoma kufanya shughuli za uchinjaji wakishinikiza kampuni ya nyama ya taifa TMC kuwalipa malimbikizo ya mshahara na stahiki zao kwa kipindi cha miezi mitatu na kusababisha uhaba mkubwa wa kitoweo cha nyama kwa wakazi wa jiji la Dodoma.

Mgomo huo ulioanza majira ya alfajiri muda ambao shughuli za uchinjaji na usambazaji wa nyama zinafanyika ambapo wafanyakazi wa machijio hayo wanasema wameamua kuchukua hatua hiyo ili kushinikiza walipwe madai yao.

Aaron Luziga ni mtendaji mkuu wa TMC anakiri kuwepo kwa madai ya wafanyakazi hao ambapo anasema hali hiyo imechangiwa na kushuka kwa uzalishaji na mabadiliko ya mfumo wa biashara ya chakula hasa kwa wateja kutoka nchi za ughaibuni.

Kufuatia mgomo huo uliodumu kwa zaidi ya saa 8 mkuu wa wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi akalazimika kwenda kuzungumza na uongozi na wafanyakazi na kuwataka kurejea kazini huku akiwaahidi serikali inashughulikia suala lao na itatoa majibu ndani ya siku saba.

Baadhi ya wafanyabiashara na wateja wa kitoweo hicho pendwa wanasema mgomo huo umewaathiri kwa kiasi kikubwa.