Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametoa rai kwa mashirika ya kimataifa yanayotekeleza miradi ya Uvuvi nchini, kuhakikisha miradi hiyo inatumika kuinua uchumi wa wavuvi na sekta ya uvuvi kwa ujumla.
Mh. Dkt. Mwinyi, amesema hayo wakati akifunga Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa Uvuvi, Bahari,na Maji ya Ndani kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), uliofanyika kwa siku 5 kwenye Ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar-es-Salaam.
"Ninatambua mradi wa Fish4ACP umefanya kazi nzuri ya kuimarisha shughuli za Uvuvi na ukuzaji Viumbe Maji kwenye mataifa 12 hapa barani Afrika hivyo ni wakati sasa kutumia somo lililopatikana kupitia mradi huo sio tu kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi bali kubadili mtazamo wa kiuchumi kwa watu wetu" Ameongeza Mhe. Dkt. Mwinyi.
Aidha Mhe. Dkt. Mwinyi amewataka Wavuvi wadogo wote waliohudhuria mkutano huo kutumia uzoefu na elimu waliyoipata kwenda kuwanufaisha wengine ambao hawakupata fursa hiyo.
"Kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu hasa ukanda wa Jangwa la Sahara mahitaji ya mazao ya Uvuvi yanatarajiwa kuongezeka maradufu kwa miongo ijayo na maji yetu sio tu yanahudumia chakula kwa mamilioni ya watu ulimwenguni bali samaki wanaotoka kwenye maji hayo ni moja ya chanzo kikubwa cha protini ambayo watu wengi wenye kipato cha chini wanaweza kuimudu" Amesisitiza Dkt. Mwinyi.
Awali akieleza yale yaliyofanyika kwa kipindi chote cha Mkutano huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kwa siku 5 zilizopita waliendesha mikutano mikubwa miwili ya Mawaziri na Maafisa wa nchi wanachama wa OACPS ambapo mkutano wa kwanza uliangazia fursa zilizopo kwenye uchumi wa Buluu ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali za Uvuvi na Maendeleo ya tasnia ya ukuzaji viumbe maji.
"Mkutano wa pili ulijikita zaidi kwenye Jukwaa la vyakula vya baharini ambapo likiangaza changamoto na fursa zilizopo kwenye mifumo ya vyakula vya bahari na maazimio ya mijadala yote yamelenga kwa mataifa haya kuwa na Uendelevu wa bahari, Maji ya ndani na Uvuvi na hivyo kuhamasisha uchumi wa buluu na uhakika wa usalama wa chakula kwa mataifa yote ya OACP" Amesema Mhe. Ulega.