Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Philip Mpango, amewataka wananchi wa Tanga kuendelea na jitihada za kulinda mazingira ili kuepukana na athari zinazoendelea kujitokeza hivi sasa ikiwemo ukosefu maji pamoja na upungufu wa chakula huku akiwasihi viongozi wa dini kuendelea kuwasisitiza waumini juu ya maandiko matakatifu yanayoagiza kuilinda dunia ikiwemo kutunza mazingira.
"Niwaombe sana na wananchi wote wa Tanga na nchi nzima tufanye kazi ya jitihada kuokoa mazingira ya nchi yetu, tusikate miti hovyo, tusiharibu vyanzo vya maji...mnasikia kule Dar es Salaam sehemu kubwa ya lile Jiji halina maji..jana nimesimama njiani pale Mkata, wananchi wanalalamika, umeme unakatika lakini ni kwa sababu mabwawa yetu hayana maji" Dkt. Philip Mpango - Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt.Mpango ameyasema hayo leo Novemba 20, 2022, mara baada ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua Jimbo katoliki Tanga.