Back to top

MSIMAMO WA PAMOJA KATIKA MAJUKWAA YA KIKANDA NA KIMATAIFA

02 July 2024
Share

Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe.Filipe Jacinto Nyusi, wamekubaliana kukuza mahusiano ya kihistoria na ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Marais hao wamefikia makubaliano hayo wakati wa mazungumzo rasmi yaliyofanyika wakati wa Ziara ya Kiserikali ya Rais Nyusi hapa nchini ambapo Rais Samia na Rais Nyusi pia wamekubaliana kuendeleza ushirikiano katika sekta ya miundombinu kama vile barabara, reli, uchumi wa buluu na anga ikiwa ni pamoja na kuanzisha safari ya ndege ya kampuni ya Air Tanzania ya moja kwa moja hadi Msumbiji.

Kwa upande mwingine, Marais hao wamekubaliana kuharakisha ujenzi wa Kituo cha Huduma cha Pamoja Mpakani, ili kuweza kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji baina ya nchi mbili hizo kupitia miradi ya pamoja na mikakati.

Tanzania na Msumbiji pia zimekubaliana kuwa na msimamo wa pamoja katika majukwaa ya kikanda na kimataifa kama vile Jumaiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola na Umoja wa Mataifa (UN).